• Hisa 174,500,000 zahamishiwa Arise B.V.

Dar es Salaam; Disemba 30, 2020: Jumatatu tarehe 28 mwezi Disemba mwaka 2020, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imeidhinisha kuhamishwa kwa hisa zinazomilikiwa na Rabobank ya Uholanzi katika Benki ya NMB kwenda Arise B.V. (‘Arise).

 

Arise B.V, ni ushirika wa uwekezaji unaoongozwa na kufadhiliwa na wawekezaji mahiri. Muungano wa wawekezaji hawa ulianzishwa mwaka 2016 na Mfuko wa Taifa wa Maendeleo wa Norway (Norfund), Benki ya Maendeleo ya Uholanzi (FMO) pamoja na   Rabobank. Kwa mantiki hiyo, Rabobank bado ni sehemu ya wamiliki/umiliki wa NMB Bank Plc kupitia Arise.

 

Lengo la Arise ni kuziendeleza taasisi za ndani za fedha na masoko yenye uwezo mkubwa wa kukua, NMB na Tanzania zikiwa miongoni mwa maeneo ya kipaumbele ya uwekezaji huo katika nchi za Afrika zilizopo kusini mwa jangwa la Sahara (SSA).

 

Kuidhinishwa kwa uhamisho wa hisa za Rabobank ndani ya Benki ya NMB kutafanya hisa 174,500,000 ambazo ni sawa na asilimia 34.9 ya hisa zote za benki ya NMB, kuhamishiwa Arise.

 

Idhinisho la CMSA linakuja baada ya ombi la hamisho la hisa la Rabobank kupata baraka kutoka mamlaka zote husika za kiudhibiti nchini.

 

Akiongea kuhusu uhamisho huo wa hisa, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi Ruth Zaipuna, amesema kuwa “kufanikiwa kukamilika kwa uhamisho wa hisa ni uthibitisho tosha wa imani ya wawekezaji katika benki yetu na Taifa kwa ujumla.”

 

Pia aliongeza kusema: “Ushirikiano kati ya Arise na NMB unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kiutendaji, kibiashara, kimuundo na kifedha ukiwa na tija ya muda mrefu kimasoko ambayo itapita matarajio ya wanahisa.”

 

Ikumbukwe kuwa NMB ni benki kubwa Tanzania kirasilimali kwa mujibu wa taarifa za fedha za robo ya tatu ya mwaka huu. Rasilimali zake ziliongezeka kwa kuweka rekodi hadi kufikia Shilingi trilioni 7.0 kutoka Shilingi trilioni 6.1 kipindi kama hicho mwaka 2019.

 

Pia NMB ni benki inayoongoza kwa kutengeneza faida kubwa nchini, baada ya kuwa imepata faida ya Shilingi bilioni 145 kipindi cha robo ya tatu ya mwaka ulioishia Septemba 30, 2020, kutoka shilingi bilioni 82 mwaka 2019.

 

Bila shaka uwekezaji huu wa muda mrefu wa Arise utasaidia matarajio ya ukuaji wa  Benki ya NMB na kuchochea ukuaji wa uchumi na ustawi wa Tanzania kupitia ongezeko la huduma jumuishi za kifedha, na ukuaji wa sekta za biashara ndogo na za kati, kampuni za kijasiriamali na kilimo.

 

Benki ya NMB inapenda kuwashukuru wanahisa wote, washirika wa kimkakati, wateja na wafanyakazi wake kwa kuendelea kuiamini na kuithamini.

 

MWISHO. 

 

Kuhusu NMB

NMB Bank Plc. (“NMB”) ni benki kamili ya kibiashara katika Jamhuri ya muungano wa Tanzania. Kupitia idara zake nne: Wateja Wadogo na Biashara, Wateja Wakubwa na Serikali, Kilimo Biashara na Fedha za Kigeni, NMB inatoa huduma za kifedha na bidhaa kwa wateja binafsi, wakulima, wafanyabiashara ndogo, kati na wakubwa, taasisi pamoja na serikali.

NMB ina matawi 225, zaidi ya mawakala 8,000 (NMB Wakala), ATM zaidi ya 700 nchi nzima na imefika katika kila wilaya. NMB ina wateja zaidi ya milioni tatu na wafanyakazi zaidi ya 3,400.

Benki imeorodheshwa kwenye soko la hisa la Dar es Salaam na wanahisa wake wakubwa ni Arise BV yenye asilimia 34.9 ya hisa zote na Serikali ya Tanzania yenye hisa asilimia 31.8.

Kwa miaka nane mfululizo kati ya mwaka 2013 na 2020, jarida la Euromoney liliichagua NMB kuwa benki bora ya Tanzania. Pia NMB imetuzwa kama mshirika bora Afrika wa kifedha wa benki zinazofanya kazi na shirika la IFC la Benki ya Dunia na ilituzwa kama benki bora ya wateja wadogo na biashara ya Tanzania na jarida la the Banker East Africa.Na mwaka 2020 ilitatwa kua Benki salama Tanzania.

 

Kwa taarifa zaidi, wasiliana na:

Vicent Mnyanyika Ag. Head of Corporate Communications. 

 

Email: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.